NA HUSSEIN M KASSIM
Kama ni machozi, basi yanitoka kapakapa
Kama ni jitimai, sonono haliniishi
Mawazo na fikra? Ni mkururo baada ya mwingine.
Tanzia ya kifo chake baba Kennedy Atanasi Waliaula niliipokea mkesha wa tarehe 15/04/2020. Hapana shaka kuwa nitaikumbuka tarehe hii milele. Namwita baba kwa maana halisi ya mzazi. Ameniathiri pakubwa mno na pia watu wengine nchini Kenya na duniani kote. Ametuchochea baadhi yetu kufanya mambo makubwa makubwa bila shaka. Ama sio ubaba huu?
Nilikumbana na bingwa huyu kwa mara ya kwanza kupitia kitabu chake, Ndoto ya Amerika. Nilikuwa katika darasa la nne wakati huo. Weledi wake wa kifasihi katika kitabu hicho ndio uliozitekenya na kuzichochea hisia za kutaka kuwa mwandishi. Na ndicho kiini hasa naandika mpaka sasa. Ken ndiye chemchemi ya mahaba yangu ya utunzi, uandishi, fasihi na zaidi ya yote, mapenzi ya kiswahili.
Kupitia vitabu vyake vingine kama vile ndoto ya Almasi, Kufa Kuzikana na Siku Njema, moto wa kutaka kuwa bora zaidi uliendelea kuchochewa katika nafsi yangu.
Nimeishi kumsifu Ken Walibora kwa utunzi wake usio mgumu kueleweka. Daima, humtia msomaji wake kwenye ngalawa ya simulizi, akamburudisha na kumwongoa kwa lugha tamu na nyepesi hadi tamati. Ameacha pengo! Hakika, ameliacha pengo kubwa mno.
Buriani Ken wetu. Buriani bingwa. Buriani shupavu wewe mwenye staha. Buriani kielelezo changu. Buriani kielelezo chetu. Buriani mtangazaji mahiri. Buriani kwa kitengo chako katika Gazeti la Taifa Leo. Buriani baba. Buriani. Umetuwacha na ukiwa. Tunakupeza tayari. Tutakupeza daima. Tutakupeza Walibora.
Hakika umeiacha dunia ikiwa bora kuliko ulivyoipata. Umeiwacha bora zaidi aisee! Umeiwacha bora kwa kunifaa mimi. Umeiwacha bora kwa kutufaa sisi, wao na wengine. Umeiwacha bora kwa kuilisha fasihi yako komavu, taanusi, yenye ukwasi na faafu. Fasihi isiyokufa abadan! Fasihi isiyolegea. Fasihi, kiungo madhubuti cha urazini wa jamii. Lala salama. Pumzika vyema mkuu.
SALAMA WALIAULA
Umetoweka mhimili, wa’ndishi twataabika
Twasononeka kwa hili, baba yetu kaondoka
Ameng’atwa na ajali, maisha yakakatika
Kuno kustahimili, jamani ninaponzeka
Lala salama mwalimu, kwa dhati tunakupenda
Umetujaza fahamu, makini yametuganda
Fasihi twaiheshimu, tutazidi kuiponda
Nenda salama mwalimu, mbegu umeshaipanda
HUSSEIN M KASSIM
16/04/2020
NAIROBI.