KABLA SIJAOA

KABLA SIJAOA

Kabla sijaoa, nitataka kuwa na hakika kuwa anafaa kweli. Nitataka kudadisi hulka zake kwa upana. Nimpitue, halafu nimweke sawa. Nimkunje, kisha nimkunjue. Nimvae, kisha nimvue. Nimwangushe, kisha nimwinue. Nimtege, halafu nimtegue. Nitafanya yote, kwa ujinga wangu na werevu wangu, nihakikishe kuwa ninapata anayefaa.

Kabla sijaoa, nitataka kuona iwapo tunaweza kupikika katika chungu kimoja. Nitamdurusu kama kitabu nimsome kurasa zote. Wakati ninamsoma, makini yangu itapiga kambi kwenye mambo apendayo na asiyopenda, kimpacho furaha na kimkoseshacho amani, mkondo wake wa mawazo na kadhalika. Kama tutapikika chungu kimoja katika haya, ataanza kupata nafasi. Ila simaanishi kuwa ndiyo basi!

Kabla sijaoa, nitamweka kwenye mizani niudadisi utulivu na uvumilivu wake. Nitamnyima sana na kumpa kidogo. Nitamhangaisha muda mwingi na kumpa furaha kiduchu. Nitamnunia kila mara na kumfurahikia kidogo tu. Yote haya yatanisaidia kumchuja kwa misingi ya stahamala.

Kabla sijaoa, nitalipima bongo lake nione lina nini. Nitamtia darasani kwa maswali ya kipuzi na endelevu. Sitochoka kutaka kutathmini endapo bongo lake limelala ama limepevuka. Hili nitalifanya mara nyingi, lengo langu likiwa kutaka kupata mtu atakayenizalia wana wenye kujimudu. Wana ambao kando na kupasi tu skulini, wawe na uwezo wa kubaini lililo zuri na baya, miongoni mwa mambo mengi mengine.

Kabla ya kuoa, nitafanya bidii kuhakikisha kuwa ninamwoa aliye na mtazamo mmoja na wangu kuhusu dini, kuhusu ulimwengu na kuwahusu walimwengu.

Kabla sijaoa, nitatakikisha kuwa nimemchuja kutumia vigezo hivi vyote pamoja na vingine vingi.

Simaanishi kuwa ninadhamiria kumpata aliye bora katika haya yote, LA! Bila shaka, lazima wanadamu wawe na upungufu. Hakuna aliye kamili. Japo, nitajaribu sana kumvisha pete huyo ambaye atakuwa kufu yangu.

Ninaomba Mola anijaalie, aniondolee ukungu nione vizuri. Sitaki talaka kamwe, kwa kuwa sikufanya maamuzi murua wakati ninaoa. Wala sitaki mizozo ya kila mara nyumbani kwangu. Nyumbani kwangu kuwe pepo yangu ya hapa duniani. Ninataka wanangu wafaidi mahaba ya wavyele wote wawili.

Yarabi nipe hurulaini wa hapa duniani 🙏👫

Amin!

©Husni

 

This Post Has One Comment

Leave a Reply