KENYA KUONGOZA KWA SAMPULI ZA SARATANI

KENYA KUONGOZA KWA SAMPULI ZA SARATANI

Ifikapo mwaka 2030, Kenya itakuwa imepiga hatua nyingi za maendeleo. Miongoni mwazo ni miundo mbinu ya kisasa kama vile reli za umeme, majumba ya kifahari na barabara kuu zenye hadhi. Bila shaka, teknolojia itakuwa imekwea vidato sana miongoni mwa mambo mengine mengi.

Miongoni mwa mambo ninayotaraji binafsi ni idadi kubwa ya watu wanaoishi na saratani. Mwenyezi Mungu akijaalia, huenda idadi ya waathiriwa itafikia robo tatu ya umma wa Kenya. Siyo maendeleo hayo? Vitoto vitakapozaliwa, vitakuja vikiwa vimeshiba saratani. Saratani zenyewe ziwe za kila sampuli.

Ninakadiria kuwa kutawepo saratani ya macho, saratani ya nywele, saratani ya kucha, saratani ya sehemu za siri, saratani ya mifupa, saratani ya meno nahata saratani ya mdomoni. Tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika historia ya nchi hii. Nina hakika nchi yetu itadiriki kujishindia matuzo kama vile tuzo ya NOBEL kwa ajili hii. Tutazipiku nchi zote na kuwa nchi ya pekee iliyofuzu kuwa na viwango vya juu vya saratani. Itakuwa ni heko kote kote.

Tukizidi kula na kulishana nyama zilizotiwa kemikali hatari, mbona tusipate saratani? Mbona? Tukizidi kubugia pombe bila ya makini, kula maboga yaliyokuzwa na kemikali, kula kuku ghushi na mayai haya yasiyoweza kuanguliwa vifarangara, tutakosaje ufanisi huu wa kansa? Tutakosaje? Bila shaka tutafuzu sana.

Tukitaka kufanikisha kansa vizuri, tuvigomeni vyakula vya kiasili kama vile mihogo, viazi, mboga za kienyeji na kadhalika. Tuviwachenina kuvila hivi vya kisasa bila ya kutia hofu yoyote. Tumo kwenye usasa na tunalenga usasa mbora katika siku za halafu.

Mwisho wa kwisha, serikali italeta vifaa vingi vya kutibu na kuthibiti saratani. Isitoshe, wanasayansi watazidi kufanya uvumbuzi wa kukabiliana na saratani. Tuendeleeni kuyala mayai haya ya mjini na kuku wenye mifupa ubwabwa. Mifupa myepesi isiyotatiza kutafuna. Tulapo kuku hawa, tuifakamieni mifupa hii na kuimeza. Nakuhakikishieni kuwa mifupa hii ni hifadhi aula ya kemikali zisababishazo kansa. Asanteni Wakenya.

 

Leave a Reply