TWA TWA TWA
Vyuoni pia mchezo, kitaka alama bora

TWA TWA TWA

Na Hussein Kassim

Husni

Kazini ndicho kigezo, kuongeza mishahara

Mabosi wana uwezo, kufanya twa kila mara

Wanatiliwa vikwazo, walio kwenye ajira

Twa twa twa ndio mchezo, twa hakika inakera

 

Mturi

Kuendeleza uozo, kinyemela si hasira,

Twa inao mlazo, kulala nako kudara,

Twa ni mui mchezo, kwani unao madhara,

Twa twa twa ndio mchezo, twa hakika inakera

 

Fikirini

Vyuoni pia mchezo, kitaka alama bora,

Twatwatwa ndicho kigezo, wakati wa mhadhara,

Atatoa pendekezo, amependa yako sura,

Twatwatwa ukiitoa, alama utazipata.

 

Husni

Twa ya sasa ni uozo, kwa vikembe na vinara

Chekechea twa twa hizo, zimekolea imara

Nyimbo za mfululizo, zasifu twa kwa ishara

Twa twa twa ndio mchezo, twa hakika inakera

 

Laventa

Twa twa mekuwa uozo, insi wakosa ubora

Ajira sasa ni bezo, twa twa mekuwa ukora

Kanisani twa mchezo, wa’mini kwiga madhara

Twa twa twa ndio mchezo, twa hakika inakera

 

This Post Has 2 Comments

  1. Edwin Musumba

    Swafi. Twa twa twa imekuwa kigezo cha kila kitu…

     

Leave a Reply