UJANA KAMA UKUNGU
Ujana maji ya moto, walishasema wahenga Sura huipa mvuto, ukaishi kwa kuringa Ujana kwelini moto, uakao bila kinga Ujana kama ukungu, huyeyuka liwakapo

UJANA KAMA UKUNGU

Na Ayieko Jakoyo

Ujana maji ya moto, walishasema wahenga

Sura huipa mvuto, ukaishi kwa kuringa

Ujana kwelini moto, uakao bila kinga

Ujana kama ukungu, huyeyuka liwakapo

 

Ujana uingiapo, inda mtu huzidisha

Huvuma kama upepo, huku na kule kubisha

Ila umri uzidipo, hata siha humuisha

Ujana kama ukungu, huyeyuka liwakapo

 

Ujana ni kama pombe, huilewesha akili

Huuzidisha upambe, ukajiona jabali

Ujana kama uvimbe, hujionyesha kwa mbali

Ujana kama ukungu, huyeyuka liwakapo

 

Ujana kitu hatari, hasa ukilimbukia

Waweza kutia shari, usipojikadiria

Yahitaji tafakari, la sivyo utaumia

Ujana kam aukungu, huyeyuka liwakapo

 

 

Ujana nikama donda, donda lisilofichika

Mori yaweza kupanda, ufanye yasotajika

Ujutie ukienda, ujan aukishatoka

Ujana kama ukungu, huyeyuka liwakapo

 

Ujana kweli bahari, chunga mja usizame

Hakuna alomahiri, chunga ya siku sakame

Kijana utahadhari, jichunge na ujipime

Ujana kama ukungu, huyeyuka liwakapo

 

Hapokikomonatia, nasahanishaitoa

Menginimesimulia, jukuwaninajitoa

Mafunzonishikilia, ujanasikupedoa

Ujanakamaukungu, huyeyukaliwakapo

 

©Ayieko Jakoyo:

(Malengawa Bara)

Leave a Reply