ULEMAVU WA MOYO

ULEMAVU WA MOYO

Na Hussein Kassim

“Usimfanyie masihara kwa huo upofu wake! Haipendezi…” maneno yalimtoka Latifa Baridi ambaye alielekea kuchoshwa na kuchushwa na kasumba ya Ali Baya. Rafiki yake wa dhati.  Yapata ni miezi kumi na mmoja tangu waanze kusuhubiana.

Latifa Baridi, binti mfupi mrembo. Kimo chake ni kama nusu ya urefu wa Ali Baya. Macho yake yenye weupe wa theluji yanatishia kudondoka kutokana na ukubwa wake. Rangi ya ngozi yake, maji ya kunde. Kitambaa chenye rangi ya zambarau amekitanda kichwani kikamkaa vizuri. Kimewajibika kisawasawa kuusetiri wajihi wake.

Kando yake, amesimama Baya. Mrefu wa kimo. Amekula akashiba. Vigezo vya kudhihiri udole wake ni matuta ya nyama yaliyommea kichwani, kwenye maeneo jirani ya kisogo chake. Amevaa miwani. Si miwani ya jua, wala si ya hospitalini. Hana shida yoyote ya macho. Hupenda tu kuivaa, hasa anapokuwa safarini. Haijalishi ni safari ndefu ama fupi. Labda huvaa kuongeza utanashati, kwa minajili ya kuviatua nyoyo vidada njiani. Labda… Sababu halisi, mjuwa ni yeye. Mgongoni lilikuwepo begi jeusi lenye shehena ya tarakilishi yake. Tarakilishi aliyoienzi sana.

Hapo waliposimama ni kwenye banda. Wanasubiria humo wakingoja pantoni ya kuwavusha. Wavuke waelekee nyumbani baada ya haamsini za kutwa nzima za kuzumbua riziki. Mbele ya Latifa na Ali Baya, mwanamme mmoja kifyefye alisimama. Alikuwa amesimama dede akitikisa kikombe chake cha plastiki. Kimo chake, zaidi kidogo kumpiku Latifa Baridi.

Alikitikisa kikombe kile mfululizo. Kakosa nafasi ya kupenyeza katikati ya watu akitafuta riziki. Mambo yalionekana tofauti sana siku hiyo. Si kama siku zingine. Watu hujaa bandani lakini si kama ilivyokuwa hali siku hiyo. Kama si huko kubanana kwa watu, angebatuka akapenyeza safu hadi safu, hadi safu ya mwisho. Ndani ya kikombe chake kikuukuu, ilikuwepo sarafu ya peni moja. Sijui kaipata wapi sarafu hiyo. Enzi za mapeni zilikwenda na wakoloni.

Amchokore kwa kutumia mbinu yoyote ile

“Una shilingi mia tisa nikupe hii elfu?” alitamka Ali. Swali kamwelekezea huyo mja aliyesimama mbele yao, yeye na Latifa. Kipofu alitikisa kichwa kuashiria kukana. “Haya, nipe mia nne na hamsini nikupe hii mia tano yangu… Ama huna? Mie sina sarafu za kuchezea.” Alizidi kubwata Ali.  Kwa wakati huo, meno yote nje. Alitabasamu kwa kejeli. Nia na dhamira yake, kumfanyia utani kipofu yule. Amdhalilishe. Amchokore kwa kutumia mbinu yoyote ile. Akijizatiti kama duduvule wasiochoka hadi wautoboe mti, lengo lake litatimia. Lingetimia na kuzaa matunda mazuri. Mazuri kama tufaha, tuseme.

Ali Baya alitaka sana kuona hatua ya kipofu yule baada ya maudhi yake yote. “Atabishana nami? Atanitusi? Ama atajitia tu hamnazo?” Ali aliisaili nafsi yake kwa ghibu. Akiwa kwenye hamrere zake hizo, simu yake ilikuwa hewani ikiwa imejishughulisha kunasa picha na video. Kinyakaso cha simu yake kimemwelekea maskini kipofu. Anatafuta kitoweo cha mtandaoni. Kitu cha kuwavutia watu wengi. Hupenda sana kuzitia picha na video zake kwenye mitandao ya ‘facebook’, ‘youtube’ na ‘instagram’. Hasa sana, hupenda ‘youtube’ ambayo humzalia riziki endapo ‘kazi’ alizozituma zitatazamwa na idadi kubwa ya watu. Leo hii, amepata kweli. Hajapata kitoweo tu, ni mnofu laini na mtamu. Si kitoweo cha kawaida… Maskini kipofu! Hakuwa na mwao hilo. Hilo la kunaswa na kamera…

“Zitoe upesi! Ama hutaki pesa zangu? Alifoka Baya ambaye uchu na ilhamu ya kunasa ‘mambo’ ilizidi kumpanda. Simu yake, pale pale.

Aliyepewa amri, ghafla alihisi mcheneto wa mwili. Joto lilimjaa mwilini. Kipaji chake kilifurika maji mara moja akawa anatetema kama aliyetiwa kwenye barafu. Sikwambii vibimbi vilivyommea mwilini. Hakusema lolote muda huo wote. Akilini, mawazo yalimchezea shere sana. Alielekea kuchanganyikiwa hasa. Avitoe hivyo visarafu vyake vihasabiwe? Atamwaminije lakini? Mwenyewe anajuwa kuwa hela alizo nazo mfukoni hazifiki mia tano. Hesabu zake ziko sawa bila shaka. Huhesabu anapozitoa sarafu kutoka kwenye kikombe akizielekeza mfukoni. Hajajaaliwa na macho ila ana uwezo huo. Pia zikija noti, hujuwa kuzitofautisha vizuri. Tatizo, noti zenyewe huja kwa nadra sana. Alizidi kupigana na mawazo yake.

Akaamua liwalo na liwe

Mwisho wa kwisha, alipata suluhu. Akaamua liwalo na liwe. Aliutumbukiza mkono wake wa yamini mfukoni akazitwaa hela zilizokuwa humo zote. Zote akamkabidhi Ali Baya. Bila ya kulimatia, na kwa umakini mkubwa, Baya aliupeleka mkono wake wa shimali kuhakikisha kuwa hamna kilichobaki kwenye mifuko ya maskini kipofu yule. Wa yamini ulikuwa umeshughulika kuchukua video. Kisha, alihesabu. Akahesabu tena. Jumla ya shilingi sabini na kenda. Sarafu nyingi zilikuwa za shilingi moja na shilingi tano. Kumbe hizo ndizo sadaka watoazo waja! Sadaka za kuwaauni wasiojiweza kama kipofu yule… Ndilo chumo lake la siku hiyo.

Riziki aliyotegemea kutumia kununua chajio na kisebeho cha siku iliyofuata. Riziki hiyo alifaa kuitumia kununua mavazi na mahitaji mengine mengi. Na je iwapo alikuwa na familia ya kukimu? Labda ndiyo sababu huvaa mararu. Labda ndiyo sababu hakuwa na sitara ya maguu yake; malapa ama viatu. Labda ndiyo sababu kabaki kifyefye. Hana siha maskini mtoto wa watu. Nyama za usoni zimeyeyuka. Zimeyeyuka zikamwacha kama sanamu. Ama tuseme, ni mithili ya kinyago cha kizuu. Kizuu mafupa. Hali yake taabani. Ya kutisha. Inasikitisha… yote tisa, la kumi, anatafuta riziki. Ana Imani kuwa huyo aliye mbele yake ametumwa na Jalali. Ametumwa kumfikishia riziki yake ya siku hiyo. Riziki ya shilingi mia tano!

“Chukua pesa zako. Jipange na hali yako. Hela zangu zina miradi…” Ali aliendelea kunena kivoloya. “Zangu hazichezewi! Lazima zifanyiwe kazi…” Matamshi ya masimango yalizidi kumtoka Ali Baya huku akimkabidhi maskini yule sarafu zake. Simu yake ilikuwa bado yanasa video. Aliporidhika, Baya alitomasa kwenye kiwambo cha simu yake na kuikomesha. Aliilekeza mfukoni kisha akatulia kama alivyokuwa awali. Alijitia hamnazo. Ahadi aliyompa kipofu hakuitekeleza. Akawa anangoja feri ije wavuke. Wavuke waende upande wa pili. Kufikia hapo, alihisi kuwa ametimiza asilimia tisini ya matakwa yake.

Si kengeza wala si chongo. Wala hakuna dalili zozote za macho. Sehemu za macho zimetawaliwa na mashimo tu. Mashimo mawili amabayo yamezibwa na kope. Kope zisizopepesa. Hazipepesi hata zikashughulikiwa na hodari wa madaktari wa macho. Kazaliwa hivyo. Amekuwa katika hali hiyo ya upofu toka udogoni hadi ukubwani. Machozi yalijibidiisha sana. Yalitengeza njia mbili, yakawa yanazifuata. Yalimiminika bila kupusa kwa kipindi kirefu. Yalitiririka, mengine yakamwingia kinywani. Yaliyobaki, yalifululiza yakapenyeza kwenye ukosi wa shati lake. Yalikwenda hivyo, yakamtambaa tumboni hadi kinenani. Sehemu ya mbele ya mwili wake ililoa na kurowa rovurovu. Si kwa majasho!

Subiri subiri za feri ziliendelea

Muda huo wote, hofu ilizidi kumtawala Ali Baya. Alitamani sana feri ifike waondoke. Waondoke ili asiendelee kuitazama filamu hiyo ambayo kwake, aliona kama upuzi tu. Hakuhofu watu waliokuwa hapo. Hao waliokuwa wakingoja pantoni ya kuwavusha. Iwapo walikuwa na uhasama naye, basi wangeanza mapema. Mapema alipoanza kumfanyia masihara kipofu yule.

Subiri subiri za feri ziliendelea. Nusu saa, dakika arobanne na tano, saa nzima… Hakuna feri iliyofika. Zile walizoziona majini hazikusonga. Zilibaki palepale. Ati, zote zilikuwa na hitilafu za mitambo ya injini. Wote waliokuwa hapo bandani hawakuwa na hakika ya kuvuka karibuni. Wapo waliotamauka, wakawa radhi kutafuta njia mbadala. Wengine walizidi kucharaza dua zao kwa Mterehemezi. Dua zisizoenda zikapita upeo wa macho. Dua za kuku hasa, zisizompata mwewe.

Kipofu alizidi kumimina machozi. Waliomwona walimsikitikia sana. Walimwonea kite, ila katika nyakati kama hizo, kila mtu hujitwika zigo lake. Kila mja hushughulika na masaibu yake. Utaauni vipi hali ya kuwa lipo linalokukwaza wewe? Ghafla bin vuu, usiahi ulipenya kila pembe ya banda lile. Nusura usiahi huo uvipasuwe viwambo vya masikio ya waliokuwa karibu naye, kama Latifa Baridi.

Wengi walishtuka. Wenye mazowea ya ‘mguu niponye’ walikosa nafasi za kuchomokea. Usiahi ulitoka kwa kipofu. Bila shaka, alkosa kujizuilia. Machungungu ya kufanyiwa masihara yalimchoma sana. Yalimchoma yakamfikisha hapo. Hakumbuki mara yake ya mwisho kulia hivyo. Labda ule usiahi wa vikembe baada tu ya kuzaliwa. Ama zile kwikwi za utotoni baada ya kuadhibiwa ama vitoto vinapochokozana. Siku hiyo alilia kama kitoto kidogo. Hilo likawavutiwa wote waliokuwa humo bandani.

Kwa namna fulani, wakajisahaulisha na masaibu ya kukosekana feri. Wamevuka siku nyingi. Huvuka asubuhi waendapo kazini na jioni wanaporudi numbani. Ila hilo la kipofu kulia! Hilo lilikuwa geni kwao. Kipofu huwa hapo siku zote. Hayo ni maskani yake ya siku zote. Hutafuta riziki yake hapo kila siku mchana. Ifikapo machweo, hubatuka asteaste akashika njia iendayo anakosakini. Hilo la kulia kwake waliliona la ajabu mno. Kila mmoja alinyanyua ukope kutaka kujua kilichojiri. Warefu walifaidi pakubwa mno. Walizinyosha shingo zao wakamwona vizuri kipofu ambae tabaka la sauti yake lilizidi kuongezeka. Wasiojaaliwa na kimo kirefu walitegemea umbeya tu.

“Huyu hapa! Huyuu!” Sauti zilicharaza tena hewani

“Amefanywaje Tabu? Si mazoea yake kulia! Aliyemkwaza nani? Eeh?” sauti zilitoka kotekote. Kioja hicho kikijiri, Ali Baya alikuwa ameipakata simu yake anailisha video. Amejitia hamnazo kweli. Zile hofu alizokuwa nazo awali zimemtoweka. Huwa na roho ngumu kiasi hicho. Kisha, aliuinua mkono wake wa kulia juu zaidi akawa anauzungusha hewani kuchukua video ya waja wote waliokuwa humo bandani. Mwenyewe, joho la hamnazo alilojivisha limemvaa likampwaya. Hajishengeshi na mambo ya watu. Alimpuuza Latifa ambaye alijaribu kila aliloweza kumshawishi aiweke mfukoni simu yake. Tangu mwanzo, Latifa alijaribu kumkanya ila juhudi zake hazikuelekea kufua dafu. Alifanya kadiri ya uwezo wake akakosa ufanisi. Lililosalia, atulie ajionee mkondo wa mambo. Akasimama tutwe. Anamfahamu mpenziwe kwa desturi hiyo ya kutokoma hadi amalize alichokianza. Akilianza jambo, hulitokosa hadi likaiva. Liive liwe laini. Kama sivyo, hatokuwa na amani. Atajihisi mnyonge sana. Ghalibu, likikatizwa jambo lake, hununa akakosa kumsemeza yeyote. Baadaye, hulichachisha tena mpaka maazimio yake yatimie. Huyo ndiye ali Baya.

“Huyu hapa! Huyuu!” Sauti zilicharaza tena hewani. Vidole vyote vya shahada vimemwelekea Ali Baya. “Amemsimanga!” “Amemtusi!” “Amemwibia Tabu!” Mchanganyiko wa sauti ulizidi kukita na kunoga. Ali aliidondosha simu yake mfukoni. Alisimama tisti kama jabali kubwa. Halitikiswi na upepo wala kimbunga. Alingoja mtu yeyote ajaribu kumfanyia ‘upuzi’. Misuli yake imetutumka vizuri kutokana na mazoezi ya kila siku. Ana ufahamu wa mifumo mingi ya vita. Si judo, si taekwondo, si karate… Upande mwingine, Latifa Baridi alikuwa siye tena. Hajiwezi kwa vyovyote vile. Hawafu wa kupigiwa mfano. Alifahamu vyema kuwa jambo ovu lilikuwa mbioni laja. Latifa alihofu. Alihofu sana.

“Apigwe! Atiwe adabu! Tumtengeneni jamani!” Ghafla bin vuu, Ali alikuwa yuko chini. Alilalia ubavu mmoja akawa anapokezwa mateke hapo kwenye sakafu. Alistahimili akajikaza kisabuni asiilalie tarakilishi yake iliyokuwa mgongoni. Aliipenda na kuithamini sana. Kichapo kiliendelea. Wapo waliokikanyaga kichwa, waliomsimama kifuani, wapo waliomtia mateke ya kinenani. Wengine walimkanyaga shingoni. Kila aliyepata nafasi ya kuchangia aliwajibika kisawasawa.

Alikuwa amelala chali

Waliokosa nafasi walizidi kuwatia shime wapigaji. Walishangilia. “Mtengeneze vizuri!” “Mwondoeni kutu!”

“Mtieni utu!”

Alikuwa amelala chali. Hakumbuki wala hajui kajipataje hivyo. Ameilalia tarakilishi yake aipendayo. Kipigo kiliendelea. Baya aliendelea kujigeuza angalau aulalie ubavu. Penzi la tarakilishi lilimtia uzumbukuku akawa anaijali tarakilishi kuliko nafsi yake. “Huyu ni mkaidi kweli! Anajinyoosha baada ya kipigo hicho! Tumtengeneze!”

Siku hiyo, Baya alipigwa kitutu. Alipigwa hadi ya kupigwa. Kilichomnusuru, kuja kwa feri moja. Feri iliyodaiwa kuwa ya pekee iliyokamilika kukarabatiwa. Nyingine nne zilikuwa bado majini. Hazikusonga. Ati injini zilikuwa na hitilafu… Hawakuwa na mwao kuwa palikuwapo mgomo baridi wa wafanyakazi wa hapo. Mgomo wa kuteteta kutolipwa mishahara yao kwa kipindi cha miezi mitatu. Walikuwa kwenye sakasaka za kupata haki. Ubaya ni kuwa waliokuwa kwenye banda hawakujua lolote.

Feri ilipofika, watu walimwacha Ali Baya ghafla. Wote wakasukumana kutoka bandani waking’ang’ania kuiwahi feri. Walitoka wote, wakajijaza humo hadi feri ikatapika wengine. Banda lilibaki na watu wachache sasa. Idadi ya kuhesabika; kipofu Tabu, Latifa Baridi, walinzi kadhaa na Ali Baya aliyekuwa sakafuni. Hapo alipolala, pametapakaa damu. Uso una vidonda vikubwa. Meno matano yamevunjika, matatu ya juu na mawili ya chini. Maskini! Bila kulimatia, alitiwa kwenye gari akapelekwa hospitalini. Yaliyojiri huko, fumbo…

*****

Ilipita miezi minne baada ya tukio lile la Ali Baya kupigwa. Alikuwa ana nafuu sana. Vidonda vyote alivyovipata mwilini kwenye tukio lile vilikuwa vimepona vizuri. Vilipona vyote vikabakisha makovu tu. Makovu ya kumkumbusha mkasa ule. Hatousahau maishani bila shaka. Alibakisha kidonda kimoja tu. Kidonda kisichoonekana. Kidonda kikubwa. Kidonda chenyewe hakuwa na hakika iwapo kingepona karibuni. Kilihitaji dawa mujarabu. Dawa yenyewe, aliifahamu yeye. Hapana muuguzi yeyote aliyekuwa na mwao wa dawa yenyewe. Maadamu angeipata dawa hiyo, angetulia. Akili yake ingepata uraufu. Amani ya kudumu.

Kinywani, zilikuwepo sampuli mbili za meno. Yake aliyozaliwa nayo na mengine matano ya kuficha aibu. Yalizificha zile nafasi zilizowachwa na meno yake matano yaliyovunjika. Utanashati wake ulipata dosari. Hakuweza tena kutabasamu kama alivyofanya awali. Kule kutabasamu kwa kuyaanika meno yote nje. Yote! Ikiwezekana, magego pia yalionekana. Tabasamu la kuonyesha alivyokuwa na meno mazuri. Meno yaliyopangika vizuri. Ya kutaanusi. Baada ya kipigo kile, hutabasamu hali ya kuwa midomo yote miwili imeshikana. Zaidi ya hapo, la! Labda anapolazimika kuongea. Hata azungumzapo, hutumia kiganja chake kama sitara. Maisha yake yamebadilika kweli. Yamechukua mkondo tofauti kabisa. Mkondo ambao hakuwahi kuudhania.

Inasikitisha jinsi vile kipindi kifupi huweza kubadili mambo. Hapa, nalenga mapenzi. Mahaba kati ya mwanamme na mwanamke. Kipindi kile cha miezi minne Ali akiwa hospitalini kilitosha kupata mpenzi mwingine. Latifa Baridi alikuwa tayari kwenye mapenzi na kidume kingine. Hayo ya Ali Baya yalishamtoka akilini. Alikuwa keshamsahau. Hata Ali alipomfuata akamwomba msamaha kwa dhati na kuahidi kubadilika, hilo halikufaa lolote. Latifa alishikilia kani msimamo wake wa, “Tafuta mwingine.” Hakusema Zaidi ya hapo. Hilo likamkwaza sana Ali. Lilimkosesha hamu ya kula. Akawa akila, alikula ‘iwe yawe tu.’ Vile vile, alikosa usingizi wa pono. Alilala kwa dhiki sana. Ali alitatizika kwa kipindi cha kama majuma matano. Akaanza kupata ahueni kidogo.

Siku baada ya siku, siha ya kipofu ilizidi kudorora

Pale kwenye banda ambapo alipata kipigo, dalili za yule kipofu hazikuwepo. Ali Baya alimtamani sana kipofu yule. Alitaka amwone walau kidogo tu. Alifanya bidii za kumtafuta popote alipofikiri angempata ila hakufaulu. Hakufa moyo. Kipofu naye alikuwa hatafuti tena riziki yake hapo bandani. Alilipeza banda hilo siku ile ya mkasa. Tangu siku hiyo, hajathubutu kuutua unyayo wa mguu wake hapo. Tendo lile la kufanyiwa dhihaka lilimtosha. Lilimfika pomoni akaapa kutoomba tena. Si pesa, si lolote. Aliona afadhali abaki nyumbani angoje riziki yoyote ambayo ingemfuata huko. Hakuwa radhi kupata aibu tena kama aliyoipata bandani. Nyumbani alikosakini, waliishi watu wawili; yeye na dadake mnuna. Dadake alikuwa na umri wa kama miaka thenashara. Wawili hao walitegemeana kwa hali na mali. Wakipata, walikula wote na wakikosa, walilala njaa. Hawakuwa na mtu mwingine wa aila yao. Walizaliwa wawili hivyo. Wazazi wao, marehemu. Waliiaga dunia kwenye ajali ya barabarani yapata miaka minane iliyopita.

Hali yao ilizidi kuwa ngumu kila siku. Aliyetegemewa kuleta riziki ni dadake. Alizunguka mitaani akavikusanya viporo vilivyotupwa. Ndizi zilizoiva sana, mikate iliyochacha, vyakula vya hotelini vilivyotiwa jaani na kadhalika. Hakuthubutu kuomba usaidizi wowote. Aliiheshimu nasaha ya kakake ya kutoomba.

Siku baada ya siku, siha ya kipofu ilizidi kudorora. Si kwa kuwa walikosa chakula. La! Mawazo mengi. Tukio lile la bandani lilkuwa bado likimpitikia akilini. Alinyongea sana hadi ikamlazimu dadake kumpeleka zahanatini. Alimshika kakake mkono, wakaandamana. Hiyo ilikuwa siku ya mwisho ya dada mtu kuwa na mtu wa aila yake. Wa damu yake hasa. Alisimama pembeni akayaona mauko ya kakake. Alilia sana. Alililia kwa kite ila hakuna aliyekuwa karibu kuja kumwauni kakake. Kaka yake alifumwa kisu cha shingoni, akatebwereka na kuanguka chini. Akakata roho. Muuaji wake, Ali Baya.

ingawa walinzi walimshika na mwishowe akaishia korokoroni, kwa Ali Baya, dawa mujarabu alikwishaipata. Dawa aliyoitafuta kwa muda mrefu. Kidonda chake cha moyoni kikapona. Dawa ya kidonda chenyewe, kisasi, na hakuijali miaka ishirini aliyofungwa jela kwa mauaji.

Mwisho

 

Leave a Reply